MFUMO MPYA WA USAJILI WA VYOMBO VYA MOTO (MAGARI, PIKIPIKI) NA UTOAJI WA LESENI ZA UDEREVA
Utangulizi Kuhusu Mfumo Mpya
Katika kuboresha huduma kwa walipakodi na umma kwa ujumla, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inajenga mfumo wa kisasa wa usimamizi wa kodi za ndani uitwao IDRAS. Mfumo huu unatarajiwa kuanza kutumika kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza, mfumo unahusisha moduli za Usajili na Usimamizi wa Magari na Vyombo Vingine vya Moto pamoja na Utoaji wa Leseni za Udereva na umeanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 10 Februari, 2025.
Mfumo huu unampatia nafasi mlipakodi kujihudumia mwenyewe (Self Services) kwa kuingia katika mfumo kwa kutumia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kupata mawasiliano ya ujumbe mfupi kwa njia ya simu (SMS) na barua pepe (e-mails). Kufuatia hilo taarifa za Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi zinatakiwa kuwa na taarifa sahihi ili kuwezesha mawasiliano na kupata huduma kwa ukamilifu katika mfumo huo.
Miongoni mwa taarifa muhimu za TIN zinazotakiwa kuwa na usahihi ni kama ifuatavyo:
i). Namba ya simu inayotumiwa na mwenye TIN
il). Barua pepe (email) inayotumiwa na mwenye TIN
ili). Alama za vidole na picha (Biometrics) kwa TIN za watu binafsi
iv). Taarifa nyinginezo za TIN
Aidha, ili kupata huduma mbalimbali za mfumo; mtumiaji anatakiwa kuwa na akaunti ya kumwezesha kuufikia na kuutumia mfumo kupitia Taxpayer Portal.
2.0 Huduma Katika Mfumo Mpya
Mfumo huu utakuwa na huduma mbalimbali zitakazofikika na kufanyika kwa urahisi na watumiaji watatakiwa kuzifanya wenyewe (self-services) kwa kiasi kikubwa. Miongoni mwa huduma muhimu zitakazopatikana na kufanywa na watumiaji kwa njia ya kielektroniki katika mfumo huo mpya ni kama zifuatazo:
i). Mmiliki wa gari au chombo kingine cha moto kufanya usajili (Registration) mwenyewe pindi anapoingiza gari toka nje ya nchi au kuinunua hapa nchini;
ii). Mmiliki wa gari au chombo kingine cha moto kuhamisha umiliki (Transfer of Ownership) kwenda kwa mtu au taasisi nyingine;
iii). Mmiliki wa gari au chombo kingine cha moto kubadili taarifa mbalimbali za chombo hicho pindi mabadiliko yanapotokea (change of motor vehicle particulars):
iv). Muombaji wa leseni ya udereva kufanya maombi kwa njia ya kielektroniki na kupata taarifa za kukamilika kwa ombi lake.
3.0 Mambo ya Kuzingatia ili Kutumia Mfumo Mpya
Ili kuweza kuzifikia huduma mbalimbali za usimamizi wa vyombo vya moto na leseni za udereva, TRA inapenda kuwakumbusha walipakodi na umma kwa ujumla kuzingatia yafuatayo:
i). Kuhuisha taarifa za Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ili kuwezesha kuingia katika mfumo na kupata taarifa mbalimbali juu ya huduma hizo. Tembelea tovuti ya TRA (www.tra.go.tz) kupata mwongozo wa kuhuisha taarifa za TIN kwa njia ya kieletroniki;
ii). Kufanya uhamisho wa umiliki (Transfer) wa magari na vyombo vingine vya moto ili viwe katika TIN na jina la mmiliki wa sasa na hivyo kuwezesha kutambulika na kupata huduma ikiwemo bima, stika za mapato, uhamisho wa umiliki (transfer of ownership) katika siku za usoni
Ikumbukwe kuwa kushindwa kuhuisha taarifa za TIN na kuhamisha umiliki wa gari au chombo kingine cha moto kutasababisha kushindwa kupata huduma muhimu za magari na maombi ya leseni za udereva. Mifumo imeimarishwa na ofisi zote za Mamlaka ya Mapato Tanzania zimejipanga kuwawezesha walipakodi na umma kwa ujumla kupata huduma kwa urahisi. Miongoni mwa mambo muhimu katika kuwawezesha wamiliki kupata huduma kwa urahisi ni pamoja na kufikiria utoaji wa misamaha ya riba na adhabu kwa waliochelewa kufanya uhamisho wa umiliki wa vyombo vya moto na miamala mingine.
Maelezo ya kina ya namna ya kuhuisha taarifa za TIN na kufungua akaunti katika Taxpayer Portal yanapatikana kwenye tovuti ya TRA (www.tra.go.tz).
Kwa taarifa zaidi, tembelea ofisi ya TRA iliyopo karibu nawe au wasiliana nasi kupitia:
Tovuti: www.tra.go.tz
Piga simu bure: 0800 750 075 au 0800 780 078 au 0800 110 016
WhatsApp: 0744 23 33 33
Barua Pepe: huduma@tra.go.tz au services@tra.go.tz
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Imetolewa na;
IDARA YA ELIMU KWA MLIPAKODI NA MAWASILIANO


Leave a Comment