Fahamu jinsi ya kupata Cheti cha Kuzaliwa kwa Mtoto Aliezaliwa Ndani ya Siku 90, Kwa Mtoto mwenye Siku 90 Lakini Chini ya Miaka 10 na Kupata Cheti cha Kuzaliwa Kwa Mtu Mzima Zaidi ya Miaka 10.
1. Kupata Cheti Cha Kuzaliwa kwa Mtoto Aliezaliwa Ndani ya Siku 90
Utaratibu wa kupata cheti cha kuzaliwa kwa ajili ya mtoto ambae amezaliwa ndani ya siku 90 ni wa haraka na rahisi kwa wale walio na taarifa kamili za kuzaliwa. Ili kuanza mchakato wa kuomba cheti cha kuzaliwa fuata utaratibu hapa chini
- Kizazi Hospitalini/Kituo cha Afya/Zahanati: Mzazi au mlezi atahitajika kuhakikisha amepewa “Tangazo la Kizazi” kutoka kwa mtoa huduma wa afya kabla ya kuondoka katika kituo husika.
- Kizazi Nyumbani: Iwapo mtoto alizaliwa nyumbani, mzazi au mlezi anapaswa kutoa taarifa kwa Afisa Mtendaji wa kijiji au Msajili wa Vizazi na Vifo wa wilaya ndani ya siku 90 tangu kuzaliwa. Taarifa hii itasaidia katika kupata “Tangazo la Kizazi.”
- Wasilisha “Tangazo la Kizazi”: Baada ya kupata “Tangazo la Kizazi,” mzazi au mlezi anatakiwa kuwasilisha hati hii kwa Msajili wa Vizazi na Vifo wa wilaya ambapo mtoto alizaliwa.
- Lipa Ada: Mzazi au mlezi atatakiwa kulipa ada ya usajili ambayo kwa sasa ni shilingi 8,000/=. Baada ya malipo, cheti cha kuzaliwa kitatolewa.
2. Kupata Cheti cha Kuzaliwa Kwa Mtoto mwenye Siku 90 Lakini Chini ya Miaka 10
Utaratibu huu unahusisha hatua zaidi ikilinganishwa na usajili wa ndani ya siku 90.
Fomu ya Maombi: Mzazi au mlezi anatakiwa kujaza na kuwasilisha Fomu ya Usajili wa Kizazi, B3. Fomu hii inapatikana katika ofisi za Usajili wa Vizazi na Vifo (RITA) au ofisi za serikali za mitaa.
Picha: Mzazi au mlezi anatakiwa kuambatanisha picha ya mtoto (passport size) kwenye fomu ya maombi.
Nyaraka za Ushahidi: Ili kuthibitisha taarifa za kuzaliwa, mzazi au mlezi anatakiwa kuambatanisha nyaraka kama vile:
- Pasipoti
- Cheti cha kumaliza elimu ya msingi au sekondari
- Kadi ya kliniki ya mtoto
- Cheti cha ubatizo (ikiwa inafaa)
- Barua kutoka ofisi za serikali (mfano, ofisi ya mtendaji wa kata/kijiji)
Ada ya Usajili: Baada ya kuwasilisha fomu na nyaraka, mzazi au mlezi atalipa ada ya usajili ambayo kwa sasa ni shilingi 8,000/=.
3. Kupata Cheti cha Kuzaliwa Kwa Mtu Mzima Zaidi ya Miaka 10
Utaratibu huu unahitaji umakini zaidi na nyaraka za ziada kutokana na muda mrefu uliopita.
Fomu ya Maombi: Mzazi au mlezi hujaza na kuwasilisha Fomu ya Usajili wa Kizazi, B3. “Bofya Hapa Kupakua Fomu”
Picha: Picha ya mtoto (passport size) inahitajika.
Nyaraka za Ushahidi: Mzazi au mlezi anatakiwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali kama vile:
- Kadi ya kliniki ya mtoto
- Cheti cha ubatizo (ikiwa kipo)
- Barua kutoka mamlaka za serikali (mfano, ofisi ya mtendaji wa kata/kijiji)
- Cheti cha kumaliza elimu ya msingi au sekondari
Nyaraka za Utambulisho (kwa waliozaliwa zamani): Kwa wale waliozaliwa miaka mingi iliyopita, wanatakiwa kuambatanisha nyaraka za ziada kama vile:
- Kadi ya Utaifa pamoja na Kadi ya Kura au Bima ya Afya.
- Leseni ya Gari (lazima iambatane na Kadi ya Utaifa au Kadi ya Kura).
Ada ya Usajili: Ada ya usajili kwa utaratibu huu ni shilingi 20,000/=.
Leave a Comment