Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the post-views-counter domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /www/wwwroot/net.wazaelimu.com/wp-includes/functions.php on line 6131
Mwongozo wa Jinsi ya Kupata Pasipoti na Hati za Kusafiria

Mwongozo wa Jinsi ya Kupata Pasipoti na Hati za Kusafiria

Fahamu Jinsi ya Kupata Pasipoti na Hati za Kusafiria. Mwongozo huu ni nyenzo muhimu ya kumsaidia mwombaji wa pasipoti au Hati ya kusafiria kufahamu vigezo na hatua mbalimbali anazotakiwa kufuatwa ili kupata huduma husika. Aidha, mwombaji ambaye anahitaji maelezo ya ziada au ufafanuzi zaidi kuhusu huduma ya pasipoti na masuala mengine ya kiuhamiaji anaweza kufika katika Ofisi yoyote ya Uhamiaji iliyo karibu naye.

AINA ZA PASIPOTI

Idara ya Uhamiaji inatoa aina mbalimbali za Pasipoti kwa raia wa Tanzania ambazo ni; Pasipoti ya kawaida (Ordinary Passport), Pasipoti ya kiutumishi (Service Passport) na Pasipoti ya Kidiplomasia (Diplomatic Passport).

1. PASIPOTI YA KAWAIDA (ORDINARY PASSPORT)

Pasipoti hii hutolewa kwa raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madhumuni ya kusafiri nje ya nchi. Pasipoti hiyo hutolewa, ikiwa na uhai wa muda wa miaka kumi. Aidha, ikiisha muda wake wa matumizi au kujaa, mmiliki anaruhusiwa kuomba pasipoti nyingine. Rangi ya pasipoti hii ni bluu (sky blue). Pasipoti hii anaweza kuitumia kwenda nchi zote duniani.

2. PASIPOTI YA KIUTUMISHI (SERVICE PASPORT)

Pasipoti hii hutolewa kwa raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amabaye ni kiongozi katika Serikali ambaye ameainishwa kwenye Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria, Sura ya 42. Pasipoti hiyo hutolewa ikiwa na uhai wa muda wa miaka mitano na mwonekano wake ni rangi ya kijani. Pasipoti hii anaweza kuitumia kwenda nchi zote duniani.

3. PASIPOTI YA KIDIPLOMASIA (DIPLOMATIC PASSPORT)

Pasipoti hii hutolewa kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni kiongozi katika Serikali mwenye hadhi maalum ya kupewa Pasipoti hiyo kama ilivyo ainishwa kwenye sheria ya Pasipoti na Hati za Safari Sura 42. Pasipoti hiyo hutolewa ikiwa na uhai wa muda wa miaka mitano na mwonekano wake ni raingi nyekundu. Pasipoti hii anaweza kuitumia kwenda nchi zote duniani.

ANGALIZO

Mwombaji aliyepewa Pasipoti ya kiutumishi au kidiplomasia, endapo atastaafu au kujiuzulu au kuondolewa kwenye nafasi iliyompa sifa ya kupatiwa pasipoti hiyo, atapaswa kuirudisha kwenye mamlaka husika (Uhamiuaji) na endapo atahitaji kusafiri nje ya nchi, atatumia pasipoti ya kawaida (Ordinary Pasipoti).

AINA ZA HATI ZA SAFARI

Idara ya Uhamiaji Tanzania inatoa aina tatu za hati za safari ambazo ni; Shahada ya Dharura ya kusafiria, Hati ya Utambulisho (Certificate of Identity) na Hati ya kusafiria ya Mkutano wa Geneva (Convention Travel Document).

1. HATI YA KUSAFIRIA YA DHARURA (EMERGENCY TRAVEL DOCUMENT)

Hati hii hutolewa kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ana safari ya dharura lakini hajakamilisha taratibu za kupata pasipoti ya kawaida. Aidha hati hutolewa pia kwa raia wa Tanzania anayetaka kusafiri nje ya nchi na hawezi kupata pasipoti kwa muda muafaka. Vilevile hati hii hutolewa kwa raia aliye kwama nje ya nchi au anayerudishwa nchini kutoka nchi za nje.

Hati hii hutumika mara moja tu, yaani kwenda katika nchi husika na kurudi nchini. Mara baada ya kurejea nchini, mmiliki ataikabidhi shahada hii kwa Afisa Uhamiaji katika kituo husika cha kuingilia nchini.

Shahada hii ya dharura hutolewa katika Ofisi zote za Uhamiaji za mikoa na Ofisi zote za Uhamiaji za Wilaya.

2. HATI YA UTAMBULISHO (CERTIFICATE OF IDENTITY)

Hati hii hutolewa kwa mtu ambaye siyo raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye hawezi kupata pasipoti kutoka katika nchi ambayo ni raia au ambaye hana uraia wa nchi yeyote kwa madhumuni ya kusafi nje ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania. Hati hii hutolewa katika Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu na Afisi Kuu Zanzibar.

3. HATI YA KUSAFIRIA YA MKUTANO WA GENEVA (GENEVA CONVENTION TRAVEL DOCUMENT).

Hati hii hutolewa kwa mkimbizi aliyepewa hifadhi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ana hitaji kusafiri nje ya nchi baada ya kukidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria Wakimbizi ya Mwaka 1998. Hati hii hutolewa katika Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu na Afisi Kuu Zanzibar baada ya kupata uthibitisho kutoka Idara ya wakimbizi.

JINSI YA KUOMBA PASIPOTI

1. Mtu anayetaka kuomba Pasipoti ya Tanzania anatakiwa kutembelea tovuti ya Idara ya Uhamiaji (www.immigration.go.tz), kisha anakwenda kwenye e-Services, ana bofya Online Passport Application Au anaweza kuipata fomu hiyo moja kwa moja kwa kubofya linki ifuatayo: https://eservices.immigration.go.tz/online/passport

2. Baada ya kuingia kwenye ukurasa wa maombi ya pasipoti, mwombaji ambaye ndio anaanza kujaza fomu yake atachagua OMBI JIPYA. Ikiwa mwombaji alishaanza kujaza fomu akaishia katika hatua fulani, anapotaka kuendelea atachagua ENDELEZA OMBI. Na ikiwa alishajaza na kukamilisha fomu yake, na sasa anataka kuangalia maendeleo ya ombi lake atachagua ANGALIA OMBI.

3. Kwa mwombaji anayeanza kujaza fomu yake, baada ya kuchagua OMBI JIPYA, katika ukurasa utakaofunguka atahitajika kufanya uchaguzi wa Aina ya Ombi. Ikiwa mwombaji hakuwahi kuwa na pasipoti atachagua OMBI JIPYA. Ikiwa mwombaji aliwahi kuwa na pasipoti na sasa imejaa, au alikuwa na pasipoti ya zamani sasa anahitaji pasipoti ya kielektroniki atachagua PASIPOTI IMEJAA/IMEISHA MUDA WAKE/KUPATA PASIPOTI NYINGINE.

4. Ikiwa mwombaji alipoteza pasipoti yake ya awali atachagua PASIPOTI ILIYOPOTEA na ikiwa pasipoti yake imeharibika au kuungua moto atachagua PASIPOTI ILIYOHARIBIKA/KUUNGUA MOTO;

5. Baada ya kuchagua aina ya ombi, mwombaji atajaza taarifa zake kwa usahihi na ukamilifu;

6. Kisha ataambatisha picha na viambato vinavyohitajika;

7. Baada ya kukamilika kwa hatua zote, mwombaji atapatiwa fursa ya kuhakiki taarifa alizojaza na baada ya uhakiki atatakiwa kuthibitisha taarifa hizo kwa kuweka alama ya vema (tick) kwenye chumba cha fomu kwenye mahali pa Tamko “Declaration”;

8. Baada ya kuthibitisha taarifa za mwombaji, atapatiwa Namba ya kumbukumbu ya malipo (control number) ya Tsh 20,000. Kwa mwombaji aliyeomba akiwa nje ya nchi atapatiwa ada yote kwa mkupuo ambayo ni USD 90;

10. Baada ya kulipia, mwombaji atachapisha fomu yake na kuiwasilisha pamoja na vielelezo vingine katika Ofisi ya Uhamiaji ya mkoa iliyo karibu naye au ofisi ya Uhamiaji Kurasini au Afisi kuu Zanzibar;

11. Mara baada ya Afisa kujiridhisha na vielelezo na maelezo ya mwombaji, atampatia Namba ya kumbukumbu ya malipo (control number) ya Tsh 130,000;

12. Baada ya mwombaji kulipia, ombi lake litapokelewa na atatakiwa Kwenda kupiga picha na kuchukuliwa alama za vidole (fingerprints);

13. Baada ya kukamilisha hatua hiyo mwombaji atajulishwa siku ambayo atatakiwa kufika Ofisini kuchukua pasipoti yake.

ZINGATIA

Mwombaji anatakiwa kuwa makini wakati wa kuchagua Aina ya Ombi kwa kuwa viwango vya ada vinatofautiana kulingana na uchaguzi husika. Mwombaji yeyote atakayefanya uchaguzi kimakosa, hatokuwa na nafasi ya kuja kudai ada ya mwanzo ili kulipia uchaguzi tofauti. Badala yake atalazimika kujaza fomu nyingine kwa usahihi

JINSI YA KUFANYA MALIPO

Malipo yote ya huduma hii yafanyike kupitia Namba ya kumbukumbu (Control Number) iliyotolewa;

Malipo yanaweza kufanyika kwa njia ya simu ya mkononi au kwa njia ya benki;

Malipo yazingatie aina na kiasi cha fedha kilichoainishwa kwenye Namba ya kumbukumbu ya malipo.

Malipo ya huduma iliyoombwa nje ya nchi yafanyike kwa kutumia kadi (Mastercard/Debit card) au kwa njia ya benki (Swift Transfer)

ZINGATIA

Mwombaji hapaswi kumkabidhi Afisa fedha za malipo ya ada ili amlipie.

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA WAKATI WA KUJAZA FOMU

Kabla ya kuanza kujaza fomu, hakikisha unavyo vielelezo vyote vinavyohitajika.

Taarifa za mwombaji zijazwe kwa herufi kubwa.

Hakikisha taarifa za mwombaji wa pasipoti zinajazwa kwa usahihi na kwa ukamilifu;

Hakikisha majina yanayojazwa yanafanana na yale yaliyomo kwenye cheti cha kuzaliwa au kiapo cha kuzaliwa mwombaji;

Ikiwa majina yanatofautiana kiapo cha kawaida au au kiapo cha kubadili majina (Deedpoll) kitahitajika kutegemeana na utofauti wa majina uliopo.

Endapo mwombaji atagundua tatizo lolote kwenye taarifa alizojaza baada ya kuwa amekamilisha na kuchapa (print) fomu yake, atapaswa kurekebisha taarifa husika kwa kutumia kalamu ya wino na kisha kusaini mbele ya taarifa mpya iliyoingizwa;

Mwombaji ambaye Pasipoti yake itabainika kuwa na makosa baada ya kuchapwa, atawajibika kujaza fomu nyingine na kulipa ada kamili ya pasipoti (Tsh. 150,000/-) ili aweze kupatiwa pasipoti nyingine;

Malipo ya ada ya pasipoti yafanywe kwa kutumia namba husika ya kumbukumbu ya malipo (Control Number) iliyotolewa baada ya kukamilisha kujaza fomu;

Baada ya fomu kukamilika na kuchapwa (printed) mwombaji atapaswa kukamilisha taarifa katika kifungu cha 7 na cha 9. Kifungu cha 7 kitajazwa na wadhamini wa mwombaji na kutiwa sahihi. Na kifungu cha 9 kitajazwa na Hakimu, Jaji, Wakili au Kabidhi Wasii (mmojawapo) na kisha atagonga muhuri.

Mwombaji ambaye atalazimika kutumia kiapo cha kuzaliwa badala ya cheti cha kuzaliwa, ahakikishe kiapo husika kinaambatishwa na stempu ya ushuru kama inavyoelekezwa na Sheria ya Viapo;

Mwombaji ambaye ana umri chini ya miaka 18, wakati wa kuwasilisha fomu yake Ofisini atapaswa kufika na mzazi au mlezi wake anayetambulika kisheria.

VIAMBATO VYA MWOMBAJI WA PASIPOTI

Mwombaji wa pasipoti anapaswa kuambatisha nyaraka za kuthibitisha uraia wake na pia nyaraka za kuthibitisha shughuli anazofanya. Aidha, ikiwa mwombaji hana shughuli yoyote anayofanya atalazimika kuthibitisha safari aliyonayo.

VIAMBATO VYA MSINGI

Cheti cha kuzaliwa mwombaji au cheti cha Tajnisi;

Cheti au kiapo cha kuzaliwa mmoja wa mzazi wa mwombaji au cheti cha Tajnisi;

Kitambulisho cha Taifa (NIDA);

Nakala ya pasipoti ya mzazi (kama anayo);

Barua ya maombi.

VIAMBATO VYA ZIADA VINAVYOWEZA KUHITAJIKA

Uthibitisho wa shughuli anazofanya mwombaji, mfano kitambulisho cha kazi na barua ya mwajiri kumtambulisha mwombaji pasipoti, Leseni ya udereva kwa wanaofanya kazi ya udereva, au leseni ya biashara au TIN Number kwa wafanyabiashara n.k AU;

Barua toka Serikali ya Mtaa inayothibiisha ukaazi wa mwombaji;

Vielelezo vya elimu kwa mwombaji anayetaka kusafiri kwa ajili ya masomo, AU

Vielelezo vya ugonjwa kwa mwombaji anayetaka kusafiri kwa ajili ya matibabu

Kwa mwombaji wa pasipoti ya kiutumishi, atahitajika kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora;

Kwa mwombaji anayeomba pasipoti ya kidiplomasia atahitajika kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

MUHIMU

Ikiwa kuna mashaka ya aina yoyote, Afisa Mdhibiti Mkuu wa pasipoti (PCO) anaweza kumtaka mwombaji kuwasilisha vielelezo vya ziada.

JINSI YA KUOMBA HATI YA DHARURA YA KUSAFIRIA

Ili kuomba Hati ya dharura ya Kusafaria mwombaji anatakiwa kufungua linki ifuatayo:

http://etd.immigration.go.tz/etd_customer/

Baada ya kuingia katika ukurasa wa maombi ya shahada ya dharura, jaza taarifa za mwombaji kwa usahihi na ukamilifu;

Ambatisha picha na viambato vinavyohitajika vya mwombaji;

Baada ya kukamilisha hatua zote chapisha fomu yako na uiwasilishe katika Ofisi ya Uhamiaji iliyo karibu nawe (isipokuwa Ofisi ya Uhamiaji Kurasini na Afisi Kuu Zanzibar). Ikiwa mwombaji yuko nje ya nchi, atawasilisha fomu yake katika Ofisi ya Ubalozi;

Mara baada ya Afisa kujiridhisha na vielelezo na maelezo ya mwombaji, atapatiwa Namba ya kumbukumbu ya malipo (control number) na atalipia kiasi cha Tsh 20,000. Ikiwa yuko nje ya nchi atalipia dola 20;

Baada ya mwombaji kulipia, ombi lake litapokelewa na kufanyiwa kazi, na mwombaji atapatiwa hati yake ndani ya masaa 24.

VIAMBATO VYA OMBI LA SHAHADA YA DHARURA

Cheti cha kuzaliwa mwombaji

Cheti au kiapo cha kuzaliwa mmoja wa mzazi wa mwombaji au cheti cha Tajnisi

Kitambulisho cha Taifa (NIDA)

Barua ya utambulisho toka Serikali ya Mtaa au Kijiji.

PASIPOTI IKIPOTEA AU KUIBIWA

Mwombaji akipoteza au kuibiwa pasipoti aliyopewa na akitaka kuomba pasipoti nyingine atalazimika kuzingatia yafuatayo;

Atatakiwa kutoa taarifa polisi kuhusiana na uptevu au kuibiwa kwa pasipoti yake.

Atatangaza kwenye magazeti mawili moja la kiingereza na Kiswahili kuhusiana na kuibiwa au kupteza pasipoti.

Atatengeneza tamko la kusheria kuhusiana na upetevu wa pasipoti yake.

Atajaza fomu ya maombi ya pasipoti nyingine kwa kufuata taratibu zote.

PASIPOTI IKIHARIBIKA

Ikiwa pasipoti itaharibika na mmiliki akawa anahitaji kupatiwa pasipoti nyingine atazingatia mambo yafuatayo:

Atajaza fomu ya maombi mtandaoni;

Atawasilisha barua ya maombi ya pasipoti nyingine inayoelezea mazingira yaliyopelekea kuharibika kwa pasipoti yake ya awali;

Atawasilisha pasipoti iliyoharibika wakati wa kuomba pasipoti nyingine.

KUTOA TAARIFA YA PASIPOTI ILIYOPOTEA AU KUIBIWA

Endapo mmiliki wa pasipoti atapoteza pasipoti yake au kuibiwa, anatakiwa kutoa taarifa kwa maandishi katika Ofisi ya Uhamiaji iliyo karibu naye. Kwa wailiopoteza pasipoti wakiwa nje ya nchi watatoa taarifa katika Ofisi ya Ubalozi. Aidha, mwombaji anaweza kutoa taarifa ya upotevu kwa kupiga namba za simu zifuatazo:

+255 262-323542 au +255 262323532. Pia, taarifa hiyo inaweza kuwasilishwa kupitia baruapepe ifuatayo: lostpassport@immigration.go.tz

Taarifa muhimu zinazotakiwa kuripotiwa ni kama ifuatavyo:

Jina kamili la mmiliki wa pasipoti;

Namba ya pasipoti (ikiwa anaikumbuka)’

Tarehe na mahali ilipopotea;

Sababu au mazingira yaliyopelekea upotevu

Aidha, mhusika ataripoti katika Kituo cha polisi ili kupatiwa Police Loss Report. Mwombaji anayewasilisha ombi la pasipoti iliyopotea anaweza kupatiwa pasipoti nyingine baada ya kuhojiwa na Afisa Mdhibiti wa Pasipoti kujiridhisha na mazingira ya upoteaji.

ADA MBALIMBALI ZA PASIPOTI NA HATI ZA SAFARI

Ada za Pasipoti na Hati za Safari ni kama zilivyo oneshwa kwenye jedwali hapa chini:

SN AINA YA PASIPOTI/HATI ADA
ILIYOOMBWA

NCHINI

ILIYOOMBWA

NCHI

NJE YA
1. Pasipoti ya Kawaida 150,000 Tsh 90 USD
3. Pasipoti ya Kiutumishi 150,000 Tsh 90 USD
4. Pasipoti ya Kidiplomasia 150,000 90 USD
5. Hati ya ya Safari Dharura 20,000 Tsh 20 USD
Certificate of Identity 10,000 N/A

PASIPOTI ILIYOPOTEA KWA MARA YA KWANZA;

S/N AINA YA PASIPOTI ADA TANZANIA

(TSH)

ADA UBALOZINI

(USD)

1. Pasipoti ya Kawaida 500,000/- 265 USD
2. Pasipoti ya Kiutumishi 500,000/- 265 USD
3. Pasipoti ya Kidiplomasia 500,000/- 265 USD
12.1.2 PASIPOTI ILIYOPOTEA KWA MARA YA PILI
1. Pasipoti ya Kawaida 750,000/- 365 USD
2. Pasipoti ya Kiutumishi 750,000/- 365 USD
3. Pasipoti ya kidipolomasia 750,000/- 365 USD
12.2 PASIPOTI ILIYO HARIBIKA
1. Pasipoti ya kawaida 300,000/- 165 USD
2. Pasipoti ya Kiutumishi 300,000/- 165 USD
3. Pasipoti ya Kidiplomasia 300,000/- 165 USD

Aidha, unaweza kuzipata ada hizo moja kwa moja kutoka kwenye tovuti yetu kupitia linki ifuatayo:

https://immigration.go.tz/index.php/application-fee-for-electronic passports-and-travel-document

TAHADHARI.

Pasipoti hii ni mali ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inaweza kuchukuliwa na Serikali wakati wowote. Ni hati ya thamani kubwa na hakuna ruhusa ya kuibadilisha kwa namna yoyote au kuacha ichukuliwe na mtu yeyote asiyestahili kuwa na Pasipoti hiyo. Kama ikipotea au kuharibiwa ni lazima taarifa kamili ipelekwe mara moja kwenye Ofisi ya Uhamiaji, Kituo cha Polisi, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulio karibu au Ubalozi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

MAWASILIANO

Ukiwa na tatizo katika kuomba pasipoti au Hati yoyote ya safari tafadhali wasiliana nasi kupitia baruapepe ifuatayo:

info@immigration.go.tz AU passporttanzania@immigration.go.tz

ANUANI YA UHAMIAJI MAKAO MAKUU

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Barabara ya Mwangosi,

S.L.P 1181,

Dodoma.

ANUANI YA AFISI KUU ZANZIBAR

Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar,

S.L.P 1354,

Zanzibar.

Leave a Comment