Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the post-views-counter domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /www/wwwroot/net.wazaelimu.com/wp-includes/functions.php on line 6131
Taarifa Kwa Umma Kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) March 2025

Taarifa Kwa Umma Kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) March 2025

 

TAARIFA KWA UMMA HATUA KALI ZA KISHERIA KUCHUKULIWA DHIDI YA WATU WOTE WANAOGHUSHI CHETI CHA KUHITIMU MAFUNZO YA JKT

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), linaendelea kutekeleza majukumu yake ya Malezi ya Vijana, Uzalishaji Mali na Ulinzi tangu kuasisiwa kwake tarehe 10 Julai, 1963.

Katika jukumu la Malezi ya Vijana, JKT linaendesha Mafunzo kwa kundi la lazima (Mujibu wa Sheria) na Kundi la Kujitolea, ambapo Kundi la lazima Vijana hufanya Mafunzo kwa muda wa miezi mitatu na kundi la Kujitolea Vijana hufanya Mafunzo ya JKT kwa muda wa miaka miwili.

Katika Mafunzo hayo, Vijana hujengewa Uzalendo, na kufundishwa Nidhamu, Ukakamavu, Umoja wa Kitaifa, Stadi za Kazi na Stadi za Maisha ili kuweza kulijenga na kulitumikia Taifa lao.

Mafunzo hayo yanaendeshwa kwa kuzingatia Mila, Desturi na Tamaduni za kitanzania, kwa kufuata Silabi ya Mafunzo na Miongozo ya Malezi ya Vijana inayotolewa na Makao Makuu ya JKT.

Vijana hao baada ya kumaliza mkataba wa JKT kwa kundi la lazima (Mujibu wa Sheria) na Kundi la Kujitolea, hupewa cheti cha kuhitimu Mafunzo ya JKT. Cheti hicho hutolewa na Makao Makuu ya JKT kwa Vijana wote waliohitimu Mafunzo na kukidhi vigezo vya Mafunzo hayo.

Vyeti hivyo vimekuwa vikitumiwa na baadhi ya Vijana kupata ajira katika Taasisi za Kiserikali, zisizo za Kiserikali na Makampuni mbalimbali yanayohitaji kigezo cha Kijana aliyepitia Mafunzo ya JKT kama sifa muhimu kupata nafasi ya ajira sehemu hiyo.

Hivi karibuni, JKT limebaini uwepo wa vyeti vya kughushi vilivyotumika na baadhi ya vijana ambao siyo waaminifu ili kujipatia ajira katika Taasisi na Makampuni yanayohitaji watendaji waliopitia Mafunzo ya JKT.

JKT linapenda kuutaarifu Umma wa Watanzania kuwa, wale wote waliobainika na watakaobainika kughushi cheti cha JKT kwa matumizi yoyote yale hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

JKT lipo tayari kutoa ushirikiano kwa Taasisi na Makampuni yote yanayohitaji uhakiki wa vyeti vya JKT kwa watumishi wao waliopitia Mafunzo ya JKT.

Aidha, Jeshi la Kujenga Taifa linaendelea kusisitiza kuwa nafasi za kujiunga na Mafunzo ya JKT zinatolewa kila mwaka kwa vijana wa Kitanzania wenye sifa, ili wamalizapo Mafunzo ya JKT waweze kupata cheti cha kuhitimu Mafunzo ya JKT kihalali.

Pia, Jeshi la Kujenga Taifa linawakumbusha wananchi kuwa nafasi hizo zinatolewa kwa kutangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii hapa nchini,
Hivyo wananchi waepuke kutapeliwa kwa namna yoyote ile ikiwemo kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno katika simu zao, kupigiwa simu na kutakiwa kutoa kiasi fulani cha fedha ili kupata nafasi hizo.

Endapo mwananchi utapokea ujumbe wa namna hiyo, Jeshi la Kujenga Taifa linakuomba kutoa taarifa haraka katika kambi yoyote ya Jeshi au kituo chochote cha Polisi kilicho karibu na wewe, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano,
Makao Makuu ya JKT.

PAKUA PDF HAPA CHINI

Leave a Comment