Chuo Kikuu cha Dodoma kimepitia taarifa zinazosambazwa mitandaoni za madai zenye madai ya wanafunzi 400 kufutwa masomo kwa tuhuma za kudukua mfumo. Ukweli ni huu;
Jumla ya wanafunzi 170 walituhumiwa kuchezea Mfumo wa matokeo (SR2) Mwaka 2023/2024. Serikali iliunda Kikosi Kazi kilichohusisha wataaalamu wa Mifumo ya Komputa kuchunguza tuhuma hizo na kuwasilisha ripoti yao Chuo Kikuu cha Dodoma. Baada ya Chuo kupokea ripoti hiyo hatua za ndani zilianza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwapa wito watuhumiwa kuja kusikilizwa kabla ya kutoa maamuzi kwa mujibu wa Kanuni zilizopo.
Jumla ya wanafunzi 148 walisikilizwa, wanafunzi 32 hawakufika kusikilizwa. Katika wanafunzi waliosikilizwa, wanafunzi 121 walipatikana na hatia ya kuhusika kuchezea matokeo ya mitihani na kikao cha Seneti ya Chuo kupitisha kuondolewa masomoni(Discontinue). Kesi za wanafunzi 15 zinaendelea na uchunguzi zaidi. Wanafunzi wawili hawakukutwa na hatia.
Kwa mujibu wa taratibu za Chuo Kikuu cha Dodoma, mwanafunzi ambae hajaridhika na maamuzi ya Seneti anapewa nafasi ya kukata rufaa. Hivyo wanafunzi ambao hawajaridhika taratibu ziko wazi, wana fursa ya kukata rufaa kupitia mifumo iliyowekwa na Chuo.
Dirisha la rufaa hufunguliwa wiki mbili baada ya matokeo ya mitihani kutoka na kufungwa baada ya wiki mbili. Mwanafunzi ambae yupo nje ya muda, anaruhusiwa wakati wowote kuomba kukata rufaa nje ya muda.
Chuo kitaendelea kusimamia taratibu, Kanuni na Sheria za kimitihani ili kulinda ubora wa taaluma na hadhi ya Chuo, pasipo kumuonena mtu yeyote.

Leave a Comment